Thursday 18 December 2014

DOSARI SERIKALI ZA MITAA


Wakurugenzi sita wafukuzwa kazi

  • Wabainika kuzembea na kuvuruga uchaguzi
  • Ghasia: Serikali ilitimiza wajibu wake, sijiuzulu
  • CHADEMA yazidi kuweweseka na matokeo

WALIOTIMULIWA KAZI
Benjamin Majoya- Mkuranga
Abdalla Ngodu- Kaliua 
Masalu Mayaya- Kasulu 
Goody Pamba- Serengeti 
Juliua Madiga -Sengerema 
Simon Mayeye- Bunda

WALIOSIMAMISHWA KAZI
Felix Mabula- Hanang 
Fortunatus Fwema- Mbulu 
Isabella Chilumba- Ulanga 
Pendo Malabeja- Kwimba 
William Shimwela- Sumbawanga

WALIOPEWA ONYO
Mohamed Maje- Rombo 
Hamis Yuna -Busega 
Jovin Jungu -Muheza
Isaya Mngulumu- Ilala
Melchizedeck Humbe-Hai 
Wallace Karia -Mvomero

KHADIJA MUSSA NA ASNAT MKIRAMWENI
SERIKALI imewatimua wakurugenzi watendaji sita wa halmashauri kutokana na uzembe uliosababisha kutofanyika na kuvurugika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Jumapili wiki iliyopita.
Pia imewasimamisha kazi wakurugenzi wengine watano ili kupisha uchunguzi zaidi wa kiwango cha ushiriki wao katika kasoro zilizojitokeza kwenye halmashauri zao.
Aidha, wakurugenzi wengine watatu wamepewa onyo kali na kuwekwa chini ya uangalizi kubaini kama wana udhaifu mwingine ili wachukuliwe hatua zaidi.
Wakurugenzi hao walitenda makosa mbalimbali yaliyosababisha kuvurugika na kutofanyika kwa uchaguzi huo, hali ambayo inawaondolea sifa za kuwa wakurugenzi makosa hayo ni pamoja na kukosa umakini katika kuandaa vifaa hasa karatasi za kupigia kura.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Hawa Ghasia, alisema: ”Ni vema ikafahamika kwamba TAMISEMI ilitimiza wajibu wake wa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa ukamilifu kwa kutoa miongozo na mafunzo kwa watendaji wa halmashauri na mikoa ambapo iliwapa fedha ili kugharamia uchaguzi.
“Kama maelekezo, miongozo na mafunzo yangezingatiwa na kila mmoja, uchaguzi wa serikali za mitaa ungefanyika vizuri nchini kote kwa sababu wakurugenzi walikuwa wanawajibika kutambua nafasi zao kama wasimamizi wakuu wa uchaguzi huo.”
Hawa aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa serikali juu ya wakurugenzi walioshindwa kutimiza wajibu wao katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Alisema wakurugenzi hao walipaswa kufahamu uzito na dhamana waliyoibeba katika kufanikisha mchakato huo.
Kutokana na ripoti walizozipokea kuhusu masuala yaliyojitokeza katika uchaguzi huo, alisema imedhihirika kwamba wakurugenzi wa halmashauri zenye dosari walionyesha udhaifu mkubwa katika kutekeleza jukumu la usimamizi wa uchaguzi.
Alisema wakurugenzi hao walitoa taarifa za upotoshaji kuhusu maandalizi ya uchaguzi kuwa yamekamilika huku wakijua si kweli, ambapo wengine walienda mbali zaidi na kumsingizia mpigachapa mkuu wa serikali kuwa alipelekewa nyaraka kwa ajili ya kuzichana akazikosea.
Aliwataja wakurugenzi ambao uteuzi wao umetenguliwa na watapangiwa kazi za taaluma zao wakati uchunguzi zaidi ukiendelea ili kubaini dhamira ya vitendo vyao ambao ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Mkuranga, Benjamin Majoya.
Wengine ni Abdalla Ngodu (Kaliua), Masalu Mayaya (Kasulu), Goody Pamba (Serengeti), Juliua Madiga (Sengerema) na Simon Mayeye (Bunda).
Waliosimamishwa  kazi i ni Felix Mabula (Hanang’), Fortunatus Fwema (Mbulu), Isabella Chilumba (Ulanga), Pendo Malabeja (Kwimba) na William Shimwela (Sumbawanga Manispaa).
“Wakurugenzi wengine watatu wanapewa onyo kali na watakuwa chini ya uangalizi ili kubaini kama wana udhaifu mwingine ili wachukuliwe hatua zaidi,” alisema na kuwataja wakurugenzi hao kuwa ni Mohamed Maje (Rombo), Hamis Yuna (Busega) na Jovin Jungu (Muheza).
Hawa alisema wakurugenzi wengine watatu walipewa onyo na kutakiwa kuongeza umakini wanapotekeleza majukumu yao. Aliwataja kuwa ni  pamoja na Isaya Mngulumu (Ilala), Melchizedeck Humbe (Hai) na Wallace Karia (Mvomero).
Alisema TAMISEMI iliwachukulia hatua watumishi walio chini yake na alijipima kama waziri na kuona kuwa anatosha kutokana na halmashauri nyingi kufanya vizuri katika uchaguzi na kama aliyekuwa juu yake anaona hatoshi atamchukulia hatua.
Siku moja baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa na kubainika kuwepo kwa kasoro zilizosababisha kutofanyika na kuvurugika kwa uchaguzi huo, serikali iliahidi kuwasaka na kuwashughulikia watendaji waliohusika kukwamisha.
Pia alisema serikali imeanza kufanya uchunguzi kuhusiana na kasoro zilizojitokeza ili kubaini kama ilikuwa hujuma au udhaifu wa watendaji na kwamba atakayebainika hakutakuwa na msalie mtume kamwe.
Waziri huyo alitumia fursa hiyo kusisitiza kwamba kila kiongozi wa TAMISEMI ana wajibu wa kutekeleza majukunmu yake kwa weledi na uadilifu ili kuepuka kasoro zisizokuwa za lazima na kwamba hawatasita kuchukua hatua dhidi ya watakaokiuka maadili au watakaopungukiwa uwezo wa kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa.
Pia aliagiza halmashauri ya manispaa ya Ilala kumwomba radhi mpigachapa mkuu wa serikali kwa upotoshwaji uliofanywa na mmoja wa watumishi wake, aliyedai kuwa walipeleka nyaraka za uchaguzi ili zichapwe lakini zikakosewa wakati si kweli kwa sababu  zilipelekwa kwa watoa huduma binafsi.
CHADEMA WAWEWESEKA
Ikiwa siku nne baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa, CHADEMA imeanza kuweweseka kutokana na kuangushwa vibaya kwenye maeneo mbalimbali, zikiwemo ngome inazozitegemea.
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA –Zanzibar, Salum Mwalimu, alidai wameshangazwa na kitendo cha serikali kuipatia CCM taarifa kamili za uchaguzi huo huku wapinzani wakielezwa kuwa hazipo tayari.
“Tunaitaka TAMISEMI kuweka matokeo hayo hadharani yakiwa yameainishwa vizuri.  Hii ni hujuma tu kwani CHADEMA tumefanya vizuri katika uchaguzi huo. Kwa  nini kila mara CCM wanapatiwa taarifa sahihi na kwa wakati?,” alihoji.  
Mwalimu alidai hiyo inaonyesha kuna mawasiliano ya mlango wa nyuma kati ya CCM na serikali, hivyo kuiomba serikali kutangaza hadharani kuwa kama ipo kwa ajili ya CCM peke yake.
“Si matokeo ya mwaka huu tu ambayo serikali inatakiwa kuweka hadharani, bali na yale ya uchaguzi wa srikali za mitaa wa mwaka 2009, ambayo hadi sasa hayajatolewa kwa ukamilifu,” alisema. 
Alisema uchaguzi wa mwaka huu umefanyika bila mpangilio kwa kuwa  taarifa walizo nazo ni kwamba maeneo mengine haukufanyika kwa madai ya kuwepo kwa maandalizi hafifu.
“Ni jambo la kushangaza kuwa wakurugenzi wengi waliowajibishwa ni wa maeneo ambayo CHADEMA imeshinda. Wanasheria  wetu wako tayari kuwatetea wakipelekwa mahakamani kwa kuonewa,” alisema.
Alisema ni jambo la kustaajabisha serikali kusema eti miongoni mwao watapangiwa kazi nyingine kulingana na taaluma zao na kusema  inashangaza kutoogopa kuwapeleka huko kwa hofu ya kuendeleza madudu.
LHCR yalaani vurugu
KITUO cha Haki za Binadamu (LHRC), kimelaani vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa na kushauri kubadilishwa kwa Sheria ili uchaguzi huo usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, jana, Ofisa wa LHRC anayesimamia uchaguzi, Hamis Mkindi, alisema umefika wakati sasa wa NEC kusimamia uchaguzi huo badala ya Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI.
Hata hivyo, serikali imetangaza kuwa uchaguzi ujao wa serikali za mitaa utakuwa chini ya NEC kwa kuwa TAMISEMI inakabiliwa na majukumu mengi ya utendaji wa kila siku.
Mkindi alisema mbali na vurugu, changamoto zingine zilizojitokeza kwenye uchaguzi huo ni baadhi ya wananchi kupiga kura mara mbili kutokana na kutokuwepo kwa ishara kuonyesha kuwa mhusika tayari amepiga kura.
Pia alisema baadhi ya wananchi wamekuwa na uelewa mdogo kuhusiana na uchaguzi ikiwa ni pamoja na muda mfupi uliotolewa kwa ajili ya kujiandikisha, jambo ambalo limesababisha mwitio kuwa mdogo wakati wa upigaji kura.
Alitumia fursa hiyo kulipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa kushiriki kikamilifu katika kulinda raia na mali zao wakati wote wa uchaguzi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru